Skip to main content

Kenya: Mafuriko yatishia Watu waliotengwa na wenye mahitaji spesheli

Hakikisha hatua za haraka kuwalinda walio hatarini

Familia inatumia mashua baada ya kukimbia mafuriko kufuatia mvua kubwa katika mtaa wa Githurai Nairobi Kenya, Aprili 24, 2024. © 2024 AP Photo/Patrick Ngugi, File

(Nairobi) – Mamlaka nchini Kenya hazijachukua hatua za haraka kukabiliana na mafuriko yanayotokana na mvua nyingi inayonyesha nchini humo, Shirika la Human Rights Watch limesema leo. Mafuriko hayo yamesababisha vifo vya angalau watu 170, wengine laki mbili wakipoteza makazi yao, mali na miundomsingi ikiharibiwa, maisha ya watu kuhitilafiwa na kudhoofisha zaidi changamoto za kijamii na kiuchumi zinazowakumba watu.

Serikali ya Kenya ina wajibu wa kudumisha haki za binadamu kuzuia madhara yanayotabiriwa ya mabadiliko ya hali ya anga na kuwalinda watu wake janga linapotokea. Matukio ya hali ya hewa kama mafuriko ni hatari kwa watu waliotengwa na walio katika hatari,  mfano wazee, watu wenye ulemavu, watu wenye viwango vya juu vya umaskini na watu wanaoishi maeneo ya mashambani.

"Uharibifu unaoendelea unaonesha wajibu wa serikali wa kujiandaa na kuchukua hatua ya haraka kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya anga na maafa ya asili," alisema Nyagoah Tut Pur, mtafiti wa Afrika wa Shirika la Human Rights Watch. "Mamlaka za Kenya zinapaswa kuhakikisha utoaji haraka wa misaada kwa jamii zilizoathiriwa na kulinda watu walio katika hatari kubwa."

Kenya na mataifa mengi katika eneo la Afrika Mashariki yamekumbwa na mvua nyingi na isiyopungua majuma ya karibuni, huku mfumo wa hali ya anga wa El Nino ukishinda msimu wa kawaida wa mvua ya msimu. Utafiti wa karibuni unaashiria kuwa mabadiliko ya hali ya anga yanachangia hali hii. Serikali imekubali kuwa matukio ya hali hii ngumu ya anga yalitabiriwa.

Katika siku za hivi karibuni, video kwenye mitandao ya kijamii na ripoti za vyombo vya habari zinaonesha kuwa watu waliothirika walikuwa wakipata msaada kiasi au hatopata msaada wowote kutoka kwa serikali kuwasaidia kuwa salama. Vilevile ili wapate mahitaji ya msingi kama makao, huduma za matibabu, na vyakula. Vyombo vya habari viliripoti kuwa nambari za simu za kupata msaada kutoka kwa maafisa wa polisi na timu za uokoaji zilikuwa hazifanyi kazi katika baadhi ya maeneo.

Katika mipango yake ya kupambana na mabadiliko ya hali ya anga, ikiwemo Mpango Kamili wa Kitaifa wa Kukabili Mabadiliko ya Hali ya Anga 2023-2027  na mipango yake ya kuchukua hatua za dharura kunapotokea janga, Kenya ilitambua mafuriko kuwa hatari, na kuorodhesha maeneo ambayo yangeweza kuathiriwa, na ilieleza njia za kupunguza athari hizo. Kenya pia ina kitengo cha kitaifa cha Kusimamia Majanga.

Mwezi Mei 2023, Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga ya Kenya ilitoa onyo kwamba nchi ingekumbwa na mvua kubwa kutokana na El Niño kati ya Mei-Julai na Oktoba-Desemba, ikiendelea hadi mwanzoni mwa mwaka wa 2024.

Mwezi uo huo, serikali ilitangaza kuwa angalau shilingi bilioni 10 (takribani Dola za Marekani milioni 80) zingetolewa ili kusaidia katika maandalizi ya kitaifa. Sheria ya Usimamiaji Fedha za Umma ya mwaka wa 2023 inazitaka Serikali za Kaunti kutenga asilimia mbili ya bajeti yake ya kila mwaka kutumika katika kukabili majanga. Hata hivyo, serikali ilishindwa kabisa kuweka mpango kitaifa wa kukabili janga hili. Agosti mwaka wa 2023, Wizara ya Afya ilianza kushirikiana na Serikali za Kaunti kununua dawa na vifaa vya matibabu na kuanza chanjo ya kipindupindu. Lakini Oktoba, Rais William Ruto alitangaza kimakosa kuwa Kenya haitashuhudia mvua za El Nino kama ilivyokuwa imetabiriwa.

Kati ya Oktoba na Februari, watu 1781 walifariki kutokana na mafuriko kwenye kingo za mito, mafuriko na maporomoko kutokana na mvua nyingi eneo la Magharibi, Kaskazini Mashariki, eneo la Kati, na eneo la Pwani ya Kenya. Shirika la Msalaba Mwekundu pia liliripoti kuongezeka kwa magonjwa yanayosababishwa na maji kama kipindupindu na homa ya matumbo.

Haijulikana kipi kilifanyikia fedha zilizokuwa zimetengewa hatua za kukabili athari za mvua hii, huku baadhi ya vyombo vya habari vikiripoti kuwa pesa hizo zilifujwa. Mwezi Novemba, Bunge liliidhinisha fedha nyingine shilingi bilioni 8.2 (takribani Dola za Marekani milioni 60.7). Afisa mmoja kwenye Shirika la Msalaba Mwekundu aliambia Human Rights Watch kuwa Kenya inaonekana kuwa na uwezo wa kutosha na raslimali za kutosha kujiandaa kwa ajili ya mvua nyingi, ila serikali haikufanya haraka kuchukua hatua licha ya onyo kutoka kwa Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga na washirika wake.

Licha ya mafunzo haya magumu kutoka kwa mvua za msimu mwishoni mwa mwaka wa 2023 na onyo la Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga, mamlaka hazikuchukua hatua madhubuti kuepusha janga zaidi mapema mwaka wa 2024 na hazikuchukua hatua za haraka janga lilipotokea, Human Rights Watch lilisema. Haikuwa hadi Aprili tarehe 24 baada ya karibu mwezi mzima wa mvua nyingi na vifo vingi, ndipo Rais Ruto alitangaza kubuniwa kwa kamati iliyojumuisha idara mbali mbali kuongoza hatua za kuchukuliwa kukabili dharura. Viongozi wa Upinzani na viongozi wa kidini wameirai serikali kutangaza janga la mafuriko kuwa janga la Kitaifa na kuwawajibisha wale wasiowajibika.

Katika maeneo ya vitongoji jijini Nairobi kama Mathare, Mukuru kwa Njenga, na Kariobangi, athari ya mafuriko imekuwa mbaya kutokana na nyumba duni, mrundiko wa watu na miundomsingi duni ya usafi, watu wengi wakiachwa bila makao na kuibua hatari ya afya ya umma kama Maleria, kipindupindu na kuendesha. Mwanaharakati wa Haki za binadamu kwa jina Benna Buluma, maarufu kama Mama Victor, alikuwa miongoni mwa watu 10 waliofariki Aprili tarehe 4 baada ya kukwama nyumbani kwao kutokana na mafuriko.

Aprili tarehe 29, Kituo cha Haki cha Mathare kilisema kwenye mtandao wa jamii kuwa angalau watu 200 wamepoteza makazi yao na hawajapata msaada wowote kutoka kwa Serikali ya Kitaifa au Serikali za Kaunti kupata makao ya muda, chakula, na mahitaji mengine.

Mamlaka zilizopo zinafaa kufanya uchunguzi wa kina kutambua kipi kilikwenda mrama na yepi zimejifundisha, Shirika la Human Rights Watch lilisema.

Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga imetangaza kuwa mvua hii itaendelea hadi mwishoni mwa mwezi Mei.

Aprili tarehe 30, serikali ilitangaza kuwa watu wanaoishi katika maeneo hatari waondoke katika muda wa saa 48 au waondolewe kwa lazima.

Mamlaka nchini Kenya zina wajibu wa kuhakikisha hatua zote muhimu zinachukuliwa kuzuia na kumaliza masaibu ya kibinadamu yanayotokana na mafuriko yanayoendelea na kudumisha haki kwa uhai, afya bora, makazi, chakula, maji na usafi wa wale wameathiriwa. Mamlaka lazima zihakikishe hatua zinazochukuliwa ni jumuishi na zinaheshimu haki za watu.

“Serikali inafaa kuhakikisha mbinu za haraka na mwafaka kuchukua hatua janga linapotokea,” Pur alisema. “ Hili litasaidia kuhakikisha majanga aina hii siku za usoni hayakuji na madhara aina hii.”

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.

Region / Country